Jumanne 21 Julai 2026 - 01:30
Uongozi wa Nchi Umewaacha Wananchi Wake na Unasisitiza Kuikokota Lebanon Kwenye Hali Hatari Sana

Hawza/ Ali Fayyadh amesisitiza kuwa; baada ya kumalizika kwa duru ya mazungumzo mjini Roma kati ya ujumbe wa Lebanon na adui Israel, misimamo rasmi ya serikali ya Lebanon imefichuka zaidi kuliko hapo awali, na pengo kati ya uongozi wa nchi na jamii ya Lebanon, hasa wakazi wa kusini mwa nchi hiyo, limeendelea kuwa kubwa zaidi.

Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Ali Fayyadh, mbunge wa Kambi ya "Uaminifu kwa Muqawama" katika Bunge la Lebanon, alisema hayo katika hafla ya kumbukumbu iliyoandaliwa na Hizbullah kwa ajili ya shahidi Muhammad Mahdi Ali Souli, iliyofanyika katika Majmaa ya Imam Mujtaba (as), eneo la San Terez, na kuhudhuriwa na wanazuoni, viongozi mbalimbali, familia za mashahidi pamoja na idadi ya wakazi wa eneo hilo.

Alisisitiza kuwa baada ya kumalizika kwa duru ya mazungumzo mjini Roma kati ya ujumbe wa Lebanon na adui Israel, misimamo rasmi ya serikali ya Lebanon imefichuka zaidi kuliko hapo awali, na pengo kati ya uongozi wa nchi na jamii ya Lebanon, hususan jamii ya kusini mwa nchi, limeongezeka zaidi.

Aliongeza kuwa; wakati adui anaendelea kuongeza operesheni za kubomoa, kuharibu na kuchoma vijiji vilivyoathiriwa na uvamizi, viongozi wa Lebanon wanaendelea na mazungumzo yao kana kwamba hakuna kilichotokea. Aidha, licha ya kuongezeka kwa mashambulizi ya Israel, bado wanazungumzia "maendeleo" na "mambo chanya" katika mazungumzo hayo.

Fayyadh alisema: "Ni wazi kwamba uongozi huu umewaacha wananchi wake na hauna tena hisia kwa mateso ya watu wala kwa ukubwa wa uhalifu unaofanywa dhidi yao na Waisraeli. Inaonekana pia kwamba uongozi huu umekuwa sugu kwa ukosoaji, na licha ya kushindwa mara kwa mara pamoja na ushauri wa kheri unaopewa kutoka ndani na nje ya nchi, hata kutoka kwa marafiki zake, bado unasisitiza kuendelea na mkondo huo."

Aliendelea kusema: "Uongozi huu sasa hauna jambo jingine linalouhangaisha isipokuwa kupata ridhaa ya Marekani na kuhalalisha kujisalimisha mbele ya Israel kwa lengo la kuuangamiza Muqawama na kuunyang'anya silaha. Wakati huo huo, ukombozi wa ardhi, ulinzi wa wananchi, kurejea kwa wakazi katika vijiji vyao, kulinda mamlaka ya Lebanon na utulivu wa ndani, katika hesabu na misimamo yao vimebaki kuwa kaulimbiu zisizo na utekelezaji wala thamani yoyote ya vitendo."

Mbunge huyo wa Kambi ya Muqawama alisisitiza kuwa; inaonekana uongozi wa Lebanon unasisitiza kuipeleka nchi katika hali hatari sana, ambapo si ardhi wala mamlaka ya taifa vitakavyorejeshwa, bali hata utulivu wa ndani na umoja wa Walebanon vitapotea. Alisema kuwa huo ndio mpango ambao Israel imeuweka kwa umakini mkubwa, na kwamba uongozi wa Lebanon umeingia humo kwa hiari yake na kwa kubeba jukumu kamili.

Kutokana na hali hiyo, alisema tatizo kati ya Muqawama na uongozi huu limekuwa kubwa sana, njia za mawasiliano zimekatika, na uwezekano wa kufikia mwafaka umekuwa haupo tena; jambo ambalo, kwa mujibu wake, halitakuwa na mwisho mwema.

Ali Fayyadh alibainisha kuwa; Muqawama kama ilivyokuwa siku zote, uko tayari kwa uwezekano na chaguo zote, kwa kuzingatia misingi yake isiyobadilika ya kutetea nchi, kukomboa ardhi, kuhakikisha wakazi wanarejea vijijini kwao bila masharti yoyote, na kudumisha umoja wa jamii ya Lebanon.

Akizungumzia maadhimisho ya siku arobaini tangu kuuawa kishahidi Muhammad Mahdi Souli, ambaye ni mtoto wa tatu wa familia hiyo ya mashahidi, alisema: "Haijalishi tutazungumzia kwa kiwango gani ukubwa wa kujitolea huku, kujitoa huku kunahitaji azma imara, subira ya mfano wa Nabii Ayyub (as), na imani thabiti isiyoyumba. Familia ya Sayyid Abu Hussein Souli ni mfano bora wa jamii yetu na familia za mashahidi; wamepoteza nyumba zao, mali zao na kuwatoa watoto wao bora kabisa kwa ajili ya njia hii. Haya ndiyo yanayoipa njia yetu thamani ya kibinadamu na kuelezea sehemu kubwa ya nguvu ya uthabiti, Muqawama na mafanikio yetu."

Ali Fayyadh aliongeza kuwa; ndiyo sababu Hizbullah, licha ya kupokea mapigo makubwa yaliyowalenga Katibu Mkuu wake, makamanda wake na viongozi wake wengine, iliendelea kuwepo, ikabaki imara, ikajijenga upya na ikaongoza mapambano makubwa dhidi ya adui Israel.

Mbunge huyo wa Kambi ya Muqawama alisema kuwa; Hizbullah sasa, chini ya uongozi wa Katibu Mkuu wake, Sheikh Naim Qassem, inapitia moja ya hatua ngumu na tata zaidi katika historia yake kutokana na vitisho na hatari za Israel pamoja na changamoto za ndani. Alisisitiza kuwa jamii ya Muqawama, licha ya kupitia mazingira magumu, bado imesimama kwa mshikamano na uthabiti katika kushikamana na chaguo la Muqawama.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha